Na Elisha Magolanga, IUCo
ASKOFU wa Kanisa la Kiinjiri la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenburg Mdegella amesema kamwe Maaskofu hawataacha kutolea maoni masuala ya kisiasa kwani kufanya hivyo ni sawa na kujitenga na masuala nyeti yanayohusu jamii.
“Siasa ndiyo maji, shule, barabara, umeme, na matibabu ya waumini wetu.... alisema Dk. Mdegella wakati akihutubia sherehe ya kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa mwishoni mwa wiki.
Askofu Mdegella alikuwa akijibu kauli za Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Marry Chatanda na Katibu Mkuu wa CCM taifa, Yusuph Makamba ya kutaka Maaskofu kuvua majohoo iwapo wanataka kujihusisha katika siasa.
Askofu Mdegella ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho alisema kinachowasibu wanasiasa wengi hapa nchini ni kutokuwa na elimu ya kutosha hivyo kushindwa kujenga hoja za maana na zenye manufaa kwa jamii.
“Serikali ya Tanzania itegemee kupata changamoto kutoka kizazi hiki kwani wanapozalisha wasomi wategemee pia kupata changamoto...hii ni sawa na kuwasha moto na kisha kuuweka chini ya kiti walichokikalia hivyo wategemee kuungua” alieleza Askofu huyo katika sherehe ambazo pia zilihudhuriwa na Mbunge wa jimbo la Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Alisema wasomi wana jukumu la kuwa kioo na mbegu njema katika jamii wanazotoka kwa kuibadilisha jamii ili iwe na viongozi wenye hofu ya Mungu ili kuepusha tatizo la kuwa na uchafu wa Dowans, EPA, Richmond, Meremeta na Loliondo.
Hivi karibuni Chitanda alitoa kauli ya kuwapinga maaskofu na kuungwa mkono na Makamba baada ya maaskofu wa Mkoa wa Arusha kutoa tamko la kutokumtambua Meya wa Manispaa ya hiyo, Gaudence Lyimo na kuahidi kutompa ushirikiano kwa madai kwamba Serikali ya CCM ilihujumu mchakato wa uchaguzi wa Meya huyo.
Maaskofu walilaani kitendo cha polisi mkoani huo kutumia nguvu kubwa kuliko kawaida katika kuzuia maandamano hayo, na matokeo yake watu watatu walikufa na wengine zaidi ya ishirini kujeruhiwa kwa risasi za moto.
Katika hatua nyingine, Askofu Dk. Mdegella alimtaka Mbunge Msigwa kufikisha bungeni kilio cha wanafunzi juu ya urasimu wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu hapa nchini ambao unadhoofisha ubora wa elimu.
“Nakuagiza, lichukulie suala la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa uzito mkubwa, tunataka kila mwanafunzi anayedahiliwa kuingia Chuo Kikuu apate mkopo bila kujali ni maskini au tajiri, daraja la kwanza au la tatu... kama tatizo ni fedha watuambie sisi wananchi ndio wenye mamlaka ya kulitatua suala hilo” Alisema.
Naye Mchungaji Msigwa aliwataka wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kukataa kutumiwa vibaya na wanasiasa wanaolenga kujinufaisha wenyewe na kuweka pembeni maslahi ya taifa.
Alisema ni vyema wasomi wakatumia fulsa walizonazo kama nyenzo ya kulikomboa taifa kutoka katika ujinga na umaskini kwa kuwajibika kuelimisha umma masuala yanayohusu mustakabali wa kukuza uchumi wa taifa.
2naomba pia picha z malacturer zwepo ktk blog y2
ReplyDeleteahsntn sna!!!!!