Na Abela Msikula
ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) dayosis ya Iringa, Dk. Owdernburg Mdegella ameahidi kuwajengea msikiti wanajumuiya ya kiislam wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa ili kuwapunguzia adha ya kukosa mahali jirani pa kufanyia ibada.
Askofu Dk. Mdegella ambaye pia ni Mwenyekiti wa bodi ya Chuo hicho alitoa ahadi hiyo hivi karibuni wakati wa sherehe za kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza chuoni hapo.
“Nitasimamia mwenyewe ujenzi kuanzia hatua ya mwanzo hadi mwisho” alisisitiza Askofu Mdegella katika sherehe ambazo pia zilihudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Alisema hapendi kuona wanafunzi wa kiislamu chuoni hapo wakikosa mahala maalum pa kufanya ibada zao, hivyo atahakikisha anatafuta eneo jirani na chuo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hiyo ya ibada.
Akitoa maoni yake kufuatia ahadi hiyo, Kiongozi wa jumuiya ya wanafunzi wa kiislam chuoni hapo, Alli Ng’omberaye alisema watafarijika kama ahadi hiyo itatekelezwa kwani mara nyingi ni mara chache kuona ahada za majukwaani zikitekelezwa.
“Kama hilo lingekua katika utekelezaji wa haraka kama Askofu alivyotamka, tayari jumuiya ingekuwa na taarifa maana sisi ndio wahusika hawezi kufanya kitu kama hicho bila kutuhusisha” alieleza shaka yake Ng’omberaye.
Naye mchungaji Betson Sevetu ambaye ni Mshauri wa kiroho wa usharika wa chuoni hapo alisema kwa uwezo wa Askofu hilo linawezekana lakini anafikiri linaweza kuchukua muda mrefu kukamilika kwani kuna jukumu la muda mrefu la ujenzi wa kanisa chuoni hapo ambalo halijakamilika.
“Hata sisi tuna eneo tulilotengewa kwa ajili ya ujenzi
wa kanisa hapa chuoni yapata miaka saba iliyopita lakini hadi leo hata shughuli za ujenzi hazijaanza “. alisema Mchungaji Sevetu.
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na mwandishi wamesema hatua hiyo ya Askofu Dk. Mdegella kama itatekelezwa itakuwa ya kihistoria na chachu ya kuimarisha mahusiano ya watanzania bila kujali imani za kidini.
Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa kinamilikiwa na KKKT dayosisi ya Iringa. Hata hivyo kinadahili wanafunzi katika kozi mbalimbali bila kujali dini.
No comments:
Post a Comment