 |
Emmanuel Myamba,
Mmoja wa wasanii wa filamu nchini Tanzania |
Na Sango Shabani
Ni furaha ya kila Mtanzania hasa yule mpenzi wa filamu za kibongo, kwani tasnia hii imefanikiwa kupiga hatua na kuweza kujulikana ndani na nje ya Tanzania. Maendeleo haya yameanza kushusha manunuzi ya filamu toka Nigeria ambazo kwa kipindi kirefu yalikuwa yametawala katika soko la hapa nchini.
Tunawapongeza wale wachache wenye moyo wa kujitolea ambao wameifikisha tasnia hii hapa ilipo. Pamoja na mafanikio tuliyofikia, lakini bado kuna mapungufu kwenye filamu zetu ambayo kama yatarekebishwa, tasnia hii itaweza kufika mbali zaidi na kuleta changamoto ndani na nje ya Afrika.
Nchi yetu imebahatika kuwa na watu wenye vipaji vya kuigiza na kuuvaa uhusika ipasavyo. Ni mambo machache yanayo yanayoifanya tasnia hii kupoteza dira na kupewa jina la “ usanii katika sanaa ya filamu”. Hii ni sababu ya mapungufu yanayoonekana dhahiri kwenye filamu zao.
Kama ilivyo kawaida kwenye kila kilicho na mafanikio lazima kuwepo watu wenye upeo wa tofautii hasa kukwamisha suala zima la mafanikio. Hili ndio kichocheo kikubwa kinachokwamisha tasnia hii ya filamu . Wasanii wamekuwa wakilalamikia watu wa cable, yaani watu wanaofikishia watu mawimbi ya stesheni kadhaa za televisheni.
“Ikitokea mtu mmoja kati ya wale waliounganishwa na cable akaweka CD ya filamu ya kibongo au yeyote lakini kwa kuwa tunaongelea filamu za kibongo wanaweza kuona watu zaidi ya laki saba mwisho wa siku CD ,DVD ama VHS zinakosa wanunuzi sokoni” mmoja wa wadau wa tasnia ya filamu akitoa dukuduku lake kwenye kituo kimoja cha televisheni nchini.
Tatizo kubwa linalosababisha tasnia hii ipoteze uhalisia ni suala la mavazii hasa kwa waigizaji wa kike. Kumekuwa na upotoshwaji wa uhalisia kwenye mavazi. Watu wamekuwa wakishindwa kutofautisha mavazi kati ya mshichana anayeuza mwili na yule mwenye heshima zake. Ni jambo la kawaida katika filamu zetu kumuona msichana akiwa kazini lakini nguo zake zikiwa za starehe .
Tatizo lingine liko kwenye suala la uhalisia katika uigizaji. Kwa mfano, muigizaji anayepewa nafasi ya ulinzi, ni jambo lisiloingia akilini kwamba walinzi ni watu wenye vituko na utani mwingi wawapo kazini kama tunavyooneshwa kwenye filamu zetu.
Ni kuipotosha jamii kwani hata mtoto anajua kwamba mlinzi anapaswa kuwa makini na shujaa ili aweze kulinda na kupambana na uhalifu .
Ni wakati wa wasanii wa filamu kuwa makini katika kile wanachotaka jamii wajifunze kupitia wao kwani ni kazi yao kuielimisha jamii na sio kuipotosha jamii. Pia ni muda wa wasanii kujipanga na kuweka mikakati thabiti katika kuboresha tasnia hii ya filamu nchini na kuigiza kulingana na maadili ya nchi yetu sio tuige kila kitu kwa waigizaji wa nchi zingine.
Maudhui na fani ya filamu yeyote yanaleta msisimko pale waigizaji wanavyoigiza sawia na kufanana na hali halisi..
Nayo jamii na serikali inabidi isaidiane na wasaniii wa tasnia hii ya filamu katika kupambana na wale wanaojinufaisha kupitia kazi zao. Kama kulalamika, wamelalamika sana hasa kwa watu “wacable”
Serikali inashauriwa kuweka mkazo kwenye sheria za hakimiliki za wasanii na pia faini iongezwe ili iwe ngumu kwa mtu kulipa pale anapopatikana na kosa la kusambaza kazi za wasanii bila idhini ya wasanii hao.