Thursday, April 21, 2011

Waraka wa kwanza 2011 toka kwa Vitalis Maembe

 By Raphael Nyoni.

Msanii wa muda mrefu na ambaye ameweka maskani yake kule Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.Vitalis Maembe ametoa waraka. Waraka huo unaelezea mambo mbalimbali yanayoendelea nchini na baadhi ya vitu vya kufanya ili kuiboresha Tanzania.  Soma waraka Huo kama alivyoutuma kwa vyombo vya habari hapo chini.

Ndugu,

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Waziri mkuu, Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mawaziri wote wa kawaida, Mawaziri Vivuli na viongozi wote wa kiimani na kisiasa.
Heshima yenu popote mlipo!
Mswahili nawasalimia!

Mimi ni Vitali Maembe, mwanamuziki, Mswahili, Mwalimu na mtumishi mwenzenu wa waafrika.
Mnamo tarehe 03/02/2011 nilianza ya kugawa chanjo ya Rushwa, ubinafsi na uvivu kwa kutumia muziki kwa watu wote. Bila kutumwa wala kushinikizwa na mtu wala shirika, wala chama, nilianzia Bagamoyo, mitaani, viwanjani na katika shule njiani kuelekea Dodoma. Ilinichukua siku na wiki kadhaa kufika huko, namna ya kusafiri kutoka kituo mpaka kituo, ruhusa ya kufanya maonesho, vitisho, njaa vilikuwa vikwazo vikubwa. 

Hatimaye jumatano tarehe 16 februari 2011 saa nne kasoro dakika kumi natatu mimi na rafiki zangu  wawili tulifika Dodoma kituo kikuu cha mabasi. Lengo likiwa ni lilelile kuiokoa nchi yetu kwa jasho letu, akili yetu yote, moyo wetu wote na uwezo wetu wote kwa kadri tulivyoaminiwa na waswahili wenzetu, kwa kufikisha Waraka wa Chanjo wenye kurasa tano wenye ushauri na unaowaomba mawaziri na wawakilishi wafikirie namna ya kufanya marekebisho kadhaa yatakayoboresha huduma muhimu katika jamii. Ukosefu na uhaba wa huduma na haki unapelekea watanzania wengi kushiriki na kushirikishwa katika Rushwa. Hali ambayo inafanya waswahili tunatukanwa, tunatukana, kutukanishwa na kujitukanishwa, thamani ya utu wetu kutoonekana  ndani ya nafsi zetu na nje katika kuishi kwetu, kwa kifupi sisi waathirika wa rushwa tunajiona kama mifugo tu kwenu nyinyi na wakati wowote mkiamua lolote mnatufanyia, tena mmeshafanya mengi kwa manufaa yenu na mifumo yenu bila kujali uwepo wetu” 
Pia lengo lilikuwa ni kuwasilisha ujumbe kwa njia ya muziki, ujumbe ambao niliagizwa na watanzania wa kawaida.

Pamoja na kufika Dodoma hiyo jumatano ya tarehe 16 februari, hatukwenda moja kwa moja bungeni, tulipumzisha akili zetu, tukasema na njaa zetu, baada ya muafaka tarehe 17 asubuhi tulienda bungeni kuomba ruhusa kumuona Spika wa bunge ili kukabidhi waraka na kopi za albamu ya muziki ya Chanjo. Siku hiyo hatukufanikiwa kupata ruhusa, baada ya usumbufu mkubwa na vitisho getini kutoka kwa askari na wahusika wengine wa mlangoni jioni iliingia na siku ikaisha bila ruhusa. ‘haya ninayoyoyasema naamini mnayajua au mna taarifa nayo’ Hatukukubali kuondoka mpaka tulipopata ruhusa ya kukutana na msaidizi wa Spika Bw. Berege, hatukuweza kumkabidhi barua zetu sitini na nne zinazotakiwa kuwafikia mawaziri wote, wawakilishi wa vyama bungeni, spika na katibu wa bunge kwa kuwa msimamo wetu ulikuwa ni kumfikishia Spika na kumkabidhi ili kuhakikisha ujumbe unawafikia wahusika. Siku iliyofuata yaani tarehe 18 februari 2011, tulifika mapema asubuhi, mara hii tulipata ruhusa ya kuingia katika ofisi ya spika, haikuwa rahisi kuonana naye lakini tuliridhika na ukweli, hivyo tulikutana na Katibu wa spika Bw. Eliufoo na kumkabidhi ujumbe wetu aliupkea saa nne na dakika kumi na sita na akaandika na kuweka sahihi kwenye katatasi yetu nyeupe ya A4 aliyoamua kuikunja katikati kwa mapana baada ya kuandika kwa kalamu yake ya wino wa buluu kuwa amepokea ujumbe wetu.

Awamu ya kwanza ya Chanjo iliishia BASATA Baraza la Sanaa la Taifa. Watu wasiopungua Elfu Ishirini wamekwishapata Chanjo ya Rushwa, Ubinafsi na Uvivu.
Pamoja na hayo yote mpaka sasa sijapata matokeo ya ujumbe wangu Dodoma kutoka kwenu walengwa wote yaani wawakilishi wa vyama na Mawaziri wote. Spika na katibu wa bunge pia mmekaa kimya.

Sasa nawauliza hiyo ni dharau, kiburi au chuki? Na kama ni hasira au chuki mmeniwekea mimi au wananchi wenu?

Sikilizeni niwaambie,

Mnaweza kujiuliza kwanini nitumie gharama nyingi ya muda, pumzi na pesa yangu masikini kama mie na kung’ang’ania kuimba nyimbo za namna hii na kuwafikishia watu moja kwa moja, kueleka bungeni. Kwanini natumia pesa ambayo ingebidi niitumie kuwatunza wanangu wadogo nyumbani wanaosubiri msaada wangu, mimi ni mjinga? Mimi siijui raha ama sina haja ya kustarehe?  kwanini nisifanye biashara ya muziki nikawa tajiri kama hao wanamuziki wengine mnao wafagilia? Kwanini nisiwapigie kampeni niwe mmoja kati yao wanaoahidiwa viwanja ili wawadanganye masikini waswahili hali wakijua ukweli ni upi?
Sina kingine  zaidi ya mapenzi kwa nchi yangu na Afrika yangu, tumia akili na umri wako sasa kuelewa mambo mengine.

Lazima ufahamu kuwa Rushwa ndio asili ya mateso wanayoyapata watu wenu, amua leo, sema neno moja tu na watu watapona. Kwa taarifa yako mkuu, watu wanakuficha mimi nakuambia ukweli, Waswahili wanasema huwezi kuwafanya lolote wala rushwa na wezi wa nchi hii kwa kuwa wewe ni mwenzao mimi siamini hayo lakini waswahili wana misemo yao kama vile ‘Lisemwalo lipo…’ au ‘ngoma ikivuma sana…’ nk.. Wewe waswahili unawajua naomba uyatilie thamani maneno yao.
Wakuu!

Nilipoona kuwa kazi yenu ya kuongoza ni ngumu nikaona niwasaidie kurahisisha mambo fulani, lakini mnaniona mpumbavu kabisa, angalieni matusi mnayotukanwa, watu wanailaani siku waliyoenda kupiga kura kuwachagua. Mimi na waswahili wenzangu tumegundua kuwa nyinyi ugumu wa maisha haya ndio raha yenu, mateso ya watu hawa wanyonge ndio matumaini yenu ya maisha bora kwenu, na watoto wenu siku za mbeleni..

Nasema haya maneno yanayoshabihiana na lawama kwenu kwa kuwa naiona juhudi yenu ya kuwafanya watanzania wasisikie muziki wetu, muziki wa mswahili, muziki unaoeleza maisha halisi kabisa ya muafrika na kutoa ufumbuzi.

Tazama! Unawaunga mkono watu ambao wanaonekana wazi hata kwa macho ya kitoto kuwa hawana mapenzi ya kweli nasi, unatuuza watu wako kwa ushawishi wa vitu vidoogo kabisa katika maisha, Makaratasi, makaratasi tu ndiyo yanayokufanya utuone bidhaa, unampa shetani damu ya wanao! Unaiunga mkono kauli ya yule punguani mmoja wa Afrika ya kusini miaka 1980! Umesahau kabisa KIAPO chako kwa Mungu mbele ya Muumba na waswahili wote, umewasahau wazee wetu walivyoteseka na kudhalilika katika kuijenga Afrika hii? 

Nakukumbusha!
Yule punguani wa Afrika ya kusini alivyosema,
“The black is the raw material for white man. So Brothers and Sisters, let us join hands together to fight against this Black devil. By now every one of us has seen it practically that the Blacks cannot rule themselves. Give them guns and they will kill each other. They are good in nothing else but making noise, dancing, marrying many wives and indulding sex. Let us all accept that the Black man is the symbol of poverty, mental inferiority, laziness and emotional incompetence”
Je, kwa haya mnayotufanyia leo hali mkiwa wasomi na mnajua yote haya mnafikiri uongozi wenu haukubaliani na huyu bwana? Je, mnawezaje kumshawishi mswahili akawaelewa kuwa hamtumii msimamo huu kuwaongoza waswahili?

Mswahili haitaji majibu ya ahadi bali vitendo na kauli thabiti itakayompa uhuru wa kweli katika ardhi ya babaake.

Tumewapa nguvu ya kutosha itumieni kutuokoa!

Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri mkuu, Spika wa bunge la Jamhuri ya muungano Tanzania, Mawaziri wote halisi na vivuli.
Najisikia vibaya kukupa ushauri huu lakini inabidi nikupe ingawa ni aibu kwangu na watanzania wote tuliokuweka madarakani, haya mambo ilibidi uwe umeyapitia na kuyafahamu miaka mingi iliyoita na kuyatumia kama ufahamu kukurahisishia nakuiboresha kazi yako ya kuwaongoza watu ambao wameletwa kuishi Afrika ili wasipate taabu, wafurahie maisha katika nchi waliyopewa na Mungu wao.

Sikiliza Mzee wangu!
Uliamua kuiongoza afrika na ukapewa ridhaa na waafrika, usikurupuke tu ukaanza kuongoza bila kujua wapi afrika inatokea, achana na hayo mavideo za ulaya na misimamo ya kigeni, acha kujiamini na elimujoho TANZANIA NI MOJA NA HAKUTAKUJA KUWA NA TANZANIA NYINGI ZAIDI YA HII YA WASWAHILI. Tanzania ndio Afrika, Afrika ndio dunia. Kama utafanya watanzania wakuone bora basi wewe utakuwa bora kuliko viongozi wote Duniani kwakuwa watanzania ni waswahili na waswahili wanafikiria mara tatu ya mtu wa kawaida.

Tuliza akili mkubwa unisikilize.
kwa kukusaidia tu ni kwamba ujue kuwa  huna uwezo wa kuiongoza hata sehemu ndogo ya waafrika pekeyako, tena bila kujua haya nikwambiayo leo ndiyo kabisaa.
Niwie radhi mkubwa wangu kama utaona nakukosea kukwambia haya. Sikwambii haya kukushusha cheo chako, la, haya ni mapenzi tu. Nakuomba uupe heshima umri wangu, na kazi yangu kama mwanamuziki, mwalimu na mswahili kwa kusikia mafundisho yangu.

Kuna kitu kinaitwa Pan-africanism.
Ndani ya hiyo tafuta kujua kuhusu wanasiasa wake, viongozi, wanamuziki na watu wengine waliohusika na afrika kwa moyo wao wote. Mwanao nakuomba uyashike haya, kama huwezi kuhifadhi kichwani shika kalamu na uandike haya. Wengi wa hawa walifanya mambo mazuri lakini mimi nawewe hatujui nia za moyoni mwao, pia wapo wliofanya mabaya, kwa kuangalia walikoanzia mpaka wanakoishia utajua lipi linalokufaa.

Nenda ukamsome.
Nnamdi Azikiwe, Robert Mugabe, Amílcar Cabral, Muammar al-Gaddafi · Marcus Garvey, David Comissiong, Kenneth Kaunda, Samora Machel, Jomo Kenyatta, Patrice Lumumba, Thabo Mbeki, Abdias do Nascimento, Gamal Abdel Nasser,  Oliver Tambo, Kwame Nkrumah, Julius Nyerere, John Nyathi Pokela, Haile Selassie, Robert Mangaliso Sobukwe, Ahmed Sékou Touré, Abdulrahman Mohamed Babu, I.T.A. Wallace-Johnson

Usiache kumsoma.
Molefi Kete AsanteSteve BikoEdward Wilmot Blyden, John Henrik Clarke, Cheikh Anta Diop, W. E. B. Du Bois, Frantz Fanon, John G. Jackson, Yosef Ben-Jochannan, Maulana Karenga, Fela Kuti, Bob Marley, Malcolm X, Ibrahim Hussein, Zephania Mothopeng, George Padmore, Motsoko Pheko, Runoko Rashidi, Walter Rodney, Burning Spear, David G. Mailu, Henry Sylvester-Williams, Stokely Carmichael, Omali Yeshitela

Tuliza akili yako ujue wamefanya nini na wamefanyiwa nini kwaajili ya afrika yao na kwaajili yao binafsi.
Usije ukawaongoza waafrika bila ufahamu mkubwa kuhusu haya yafuatayo, hapa ndipo kuna malengo, nia, utu na heshima yetu. Kuchanganyana na kuchanganyikana.

United States of AfricaAfrocentrismKwanzaaPan-African coloursPan-African flag,  Négritude ,African nationalismAfrican socialismAfrican Century · AfricanizationKawaidaUjamaaHarambee, UbuntuZikismBlack nationalism.

Jua na uelewe kuhusu muungano, mabadiliko, umoja wetu na kudumu kwetu kama waafrika.
African UnionOrganization of African UnityUhuru MovementUNIA-ACL · African Unification FrontInternational African Service Bureau.

Hayo mambo mengine ni urembo tu, ni njia ya kutafuna rasilimali za waafrika tu. Nakuamini sana na ninaamini kuwa maneno yangu yatawasaidia watanzania na waafrika wenzangu kupitia busara zako, hayatakuwa chanzo cha wewe kunitesa au kugeuka sababu kuniua masikini mie ninayejaribu kuwakoa watanzania na waafrika wenzangu. Najua nimekupa nguvu ya kufanya lolote utakalo lakini naomba usinidhuru kwani wanangu na wapenzi wangu bado wananihidaji.

Mimi ni wanamuziki nisingependa haya yafikie huku lakini imebidi nitumie njia hii maana nimeimba sana lakini redioni hawapigi, wengi wao wanasema wanahofia utawala wenu, hautafurahia nyimbo za mafunzo, lakini labda ni uoga wao tu, nakuomba uwaruhusu basi wapige nyimbo za Vitali Maembe.

Mkuu,
Katika kuongoza yashike hayo yote lakini langu mimi ni moja tu kama si mawili, usiupe nafasi ubinafsi, ubaguzi wa rangi, dini, kabila na jinsia.

Mwisho,
Usiache muziki ukadhalilishwa, usiupromoti muziki ambao unaona wazi unawapeleka watu wako pabaya, nchi italaaniwa, Muziki mzuri ni ule unaotoa elimu njema na kuwasaidia watu, ule mwingine usiuue pia uache uwepo tu ili kutofautisha kizuri na kuzuri sana. ‘pasipo ndicho kilichopo ndicho?’
Mswahili anakutakia uongozi mwema na mafanikio katika mema!

‘Mungu ulisha ibariki Tanzania, Mungu ulisha ibariki Afrika! Tunaomba usituondolee Baraka hii!’

Thursday, April 14, 2011

Power station ya mradi wa kijiji cha chamani

Mzee Pwagu akielekea ilipo power station ya kijiji cha chamani, kijiji hicho kipo kilometa 15 kutoka ilipo power station ya mji mwema
Akifungua Mlango wa power station, pembeni ni kijana ambaye amepewa mafunzo na mzee Pwagu namna ya kutengeneza umeme na kukisimamia kituo hicho cha umeme.
Mashine ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji kama inavyoonekana.
Mashine hii inazalisha umeme wenye uwezo wa kutumika na kaya 50 katika kijiji cha chamani, lakini ni baadhi ya wanakijiji tu ndio ambao wamefikiwa na huduma hiyo
Mzee Pwagu akitoka toka power station huku akitaniana na vijana wake.

Kuelekea Mji mwema ilipo Power station ilipo...

Safari kuelekea ilipo power station
Power station inavyoonekana kwa nje
Akipima kiwango cha umeme unaozalishwa
Mtambo wa zamani kabla hajapata mafunzo toka kwa Injinia wa kijerumani jinsi ya kutengeneza umeme bila uharibifu wa mazingira

Power station
Maji yanayotoka nje baada ya kupita kwenye mota ya kuzalisha umeme. Maji haya huvunwa kutoka mtoni na kurudi tena mtoni baada ya kuzalisha umeme


Wednesday, April 13, 2011

Mzee Pwagu:Injinia wa umeme Njombe asiyefahamika

Kuna watu wengi wanaoweza kuisaidia serikali kutatua tatizo la umeme kama watatumika ipasavyo.
Bahati mbaya serikali yetu inashindwa kuwatupia macho na kuwaacha waende na vipaji vyao, 
huku taifa likizama katika giza. Mmoja wa watu wenye uwezo wa kuzalisha umeme John Mwafute,mwenye umri wa miaka 81anayefahamika zaidi kwa jina la Mzee Pwagu kutoka mjini Njombe.
Mzee Pwaguaada ya kumaliza elimu yake ya msingi alijifunza kazi ya uhunzi, kidogo kidogo akaanza kujifunza na mambo ya umeme. Alipopata ujuzi katika uhunzi na umeme, akaanza kubuni vifaa mbali mbali ambavyo vilikuwa vinamsaidia katika kazi zake za uzalishaji umeme wa maji.
Alianza kwa kuzalisha umeme wa kilowatt 1.
Baada ya kuona juhudi zake na uwezo wake wa kuzalisha umeme, akapata mafunzo zaidi kutoka kwa Godfrey Ndeo kwenye mambo ya uinjinia.
Hivi sasa anazalisha umeme wa" phase 3" ambao una uwezo wa kuendesha kiwanda, lakini anautumia katika karakana yake iliyopo Mji mwema, nje kidogo ya mji wa njombe.
Mzee Pwagu, ameamua kuwafundisha vijana juu ya ujuzi alionao. Kwa kuanza ameanza navijana walio kijiji cha Chamani, kilometa Kumi na tano kutoka njombe mjini.
Lengo lake ni kuwafikishia umeme watu wa vijijini na sehemu zote ambazo serikali imezisahau, katika huduma ya umeme.
Mafunzo kwa vijana wa kijiji cha chamani yamechukua muda wa mwaka mmoja hadi kukamilika na hivi sasa nao wanafurahia umeme uliozalishwa nao kwa msaada wa mzee Pwagu
Mzee Pwagu ni changamoto kubwa kwa "Dowans" na serikali kuhusiana na suala zima la tatizo la umeme. 

Mzee Pwagu      






"Ngoja nikuonyeshe kijana"

"Umeona mambo yangu ?Hili trela tu picha linakuja"Mzee Pwagu akimuuliza Raphael Nyoni, mwanahabari toka chuo kikuu cha Tumaini,Iringa

Hapa anasema "haya sasa twende nikupeleke kwenye power station"

Monday, April 11, 2011

Maazimisho ya 17 ya mauaji ya Kimbari 1994 Rwanda yaliyofanyika katika chuo kikuu cha Tumaini Iringa

  • Mgeni rasmi Mhe. Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda
  • Mdegela awaasa wanasiasa wa Tanzania kuacha ubinafsi
Na mpiga picha wetu Elisha Magolanga
    Mkuu wa kitivo cha sheria Renatus Mgongo, Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda Lazaro Nyalandu na Askofu wa KKKT-Iringa Dr. Owdenburg Mdegela alipowasiri chuo kikuu cha Tumaini-Iringa
    Katika ukumbi wa Multipurpose
    Askofu Mdegela akimnong'oneza waziri Nyalandu
    Wakitoa heshima ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari
    Mkuu wa kitivo cha sheria akiwakaribisha na wageni katika hafra
    Mkuu wa chuo Prof. Nicolas Bangu akifungua hafra ya maadhimisho ya mauaji ya Kimbari
    Mhadhili wa sheria akiwasilisha mada kuhusu sheria ya Kimataifa
    Mwanasaikolojia na mhadhili wa saikolojia katika chuo kikuu cha Tumaini
    Mch. Mutha Ruiza akiwasilisha mada juu ya athali za kisaikolojia zilizotokana na mauaji ya Kimbari
    Wanafunzi wakisikiliza kwa makini
    Usikivu!
    Umakini
    Ni wakati wa wasikilizaji nao kuchangia hoja, Huyu ni Mhadhili wa
    sheria akichangia hoja juu ya sheria ya kimataifa
    Mhadhili wa chuo kikuu cha Tumaini akichangia hoja juu ya
    matatizo ya kisheria yayolikumba bara la Afrika
    Godwin Kunambi akichangia hoja
    Kanyolo pia alikuwepo
    Wakiagana mwisha wa hafra